Ijumaa 20 Novemba 2026 - 22:53
Malezi ya Watoto Yaanze na Chakula cha Halali, Familia Imara Ndiyo Msingi wa Jamii Bora

Hawza/ Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania, Sheikh Hemed Jalala, amesisitiza umuhimu wa malezi bora ya watoto huku akibainisha kuwa familia imara inayojengwa juu ya misingi ya dini, maadili mema na malezi sahihi ndiyo nguzo kuu ya kuijenga jamii yenye maadili, taifa lenye utulivu na umma ulioimarika.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, akizungumza katika khutuba za Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa leo katika Msikiti wa Ghadir, uliopo Kigogo Post, jijini Dar es Salaam, Sheikh Jalala alieleza kuwa jukumu la kuwalea watoto katika misingi imara ya kiimani na kimaadili linapaswa kuanza hata kabla ya mtoto kuzaliwa. Alisisitiza kuwa wazazi wana wajibu mkubwa wa kuzingatia mwenendo wao, hususan katika masuala ya chakula wanachokula na mazingira wanayoandaa kwa ajili ya watoto wao.

Katika khutuba yake, Sheikh Jalala ambae pia ni Mkurugenzi wa Hawza ya Imaam Swa'diq (as), alieleza mambo mbalimbali yanayopaswa kuzingatiwa katika malezi ya watoto, huku akianza na suala la msingi la ulaji wa chakula cha halali.

Chakula cha halali ndio msingi wa malezi bora

Akifafanua nukta ya kwanza, Sheikh Jalala alisema kuwa mzazi anapaswa kujipamba kwa tabia ya kula chakula cha halali na kujiepusha na kila aina ya chakula kilichoharamishwa na Sheria ya Mwenyezi Mungu.

Alisisitiza kuwa; wajibu huo hauanzi baada ya mtoto kuzaliwa pekee, bali mzazi anapaswa kuuzingatia hata kabla ya kupata mtoto, kwa kuhakikisha kuwa chakula anachokula kinapatikana na kutumiwa kwa njia inayokubalika kisheria.

Aidha, alieleza kuwa chakula cha haramu si kile kinachopatikana kwa njia ya dhuluma, wizi au uporaji pekee, bali kinajumuisha pia vyakula na vinywaji ambavyo Mwenyezi Mungu ameviharamisha, kama vile nyama ya nguruwe na pombe. Hivyo, mzazi anapaswa kujiepusha navyo na kuhakikisha kuwa maisha yake yanazingatia mipaka iliyowekwa na dini.

Katika kusisitiza umuhimu wa jambo hilo, Mkurugenzi wa Hawza ya Imam Swa'diq (as) alinukuu aya ya Qur'ani Tukufu inayosema:

{ یَسۡـَٔلُونَكَ مَاذَاۤ أُحِلَّ لَهُمۡۖ قُلۡ أُحِلَّ لَكُمُ ٱلطَّیِّبَـٰتُ وَمَا عَلَّمۡتُم مِّنَ ٱلۡجَوَارِحِ مُكَلِّبِینَ تُعَلِّمُونَهُنَّ مِمَّا عَلَّمَكُمُ ٱللَّهُۖ فَكُلُوا۟ مِمَّاۤ أَمۡسَكۡنَ عَلَیۡكُمۡ وَٱذۡكُرُوا۟ ٱسْمَ ٱللَّهِ عَلَیۡهِۖ وَٱتَّقُوا۟ ٱللَّهَۚ إِنَّ ٱللَّهَ سَرِیعُ ٱلْحِسَابِ }

Wanakuuliza wamehalalishiwa nini? Sema: Mmehalalishiwa kila kilicho kizuri na vile mlivyowafundisha wanyama wawindaji kuwinda. Mnawafundisha kutokana na yale aliyokufundisheni Mwenyezi Mungu. Basi kuleni katika vile walivyowakamata kwa ajili yenu, na litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yake. Na mcheni Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.
(Suratul Ma'idah: 4).

Akielezea zaidi mafunzo yanayopatikana katika suala hilo, Sheikh Jalala alisema kuwa: Mtoto anayekulia katika mazingira ya chakula cha halali anakuwa na msingi mzuri wa kukua katika wema na maadili mema.

Katika kuthibitisha hoja hiyo, alitolea mfano wa Bibi Fatimah Zahraa (as), akieleza kuwa miongoni mwa mambo yanayoonesha utukufu wa malezi yake ni namna alivyopatikana kupitia chakula cha halali ambacho Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alikitumia.

Vilevile, Sheikh Jalala alibainisha kuwa hata ukiangalia nasaba ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.), kuanzia Nabii Adam (as), utaona kuwa wazazi waliokuwa katika mnyororo wa nasaba yake hawakuhusishwa na uchafu wa haramu. Alieleza kuwa jambo hilo ni miongoni mwa mafunzo yanayoonyesha umuhimu wa usafi na utakatifu katika misingi ya malezi na kizazi cha mwanadamu.

Sheikh Jalala aonya kuhusu mmomonyoko wa maadili miongoni mwa vijana

Katika sehemu nyingine ya khutuba yake, Sheikh Jalala alizungumzia changamoto kubwa ya mmomonyoko wa maadili inayoikabili dunia katika kipindi cha sasa, huku akieleza kuwa mazingira yanayowazunguka watoto na vijana yana ushawishi mkubwa katika kujenga au kuharibu tabia na mwenendo wao.

Alisema kuwa: Maadili yanayofundishwa katika baadhi ya mazingira ya shule na vyuo vikuu hayatoshi, kwa mtazamo wake, kuwajenga vijana katika misingi ya maadili ambayo itawawezesha kuwa watu wenye manufaa kwa familia zao, jamii na taifa kwa ujumla.

Alibainisha kuwa ingawa walimu na wazazi wanajitahidi kuwalea watoto katika mwenendo mwema, bado kuna nguvu kubwa ya ushawishi kutoka nje inayoweza kubomoa juhudi hizo na kuwavuta watoto katika mienendo inayokwenda kinyume na misingi ya dini na maadili.

Akifafanua zaidi kuhusu changamoto hiyo, Mkurugenzi huyo wa Hawza ya Imam Swa'diq (as) alisema kuwa; dunia ya leo inashuhudia vitendo vya ushoga, usagaji na ukahaba vikijadiliwa na kuwasilishwa katika baadhi ya mazingira ya kijamii kama mambo ya kawaida.

Alionya kuwa, nguvu hizo za ushawishi zinaweza kuleta changamoto kama hizo hata katika jamii ya Tanzania, hususan endapo wazazi, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla hawataweka mikakati madhubuti ya kuwalinda vijana na mabinti dhidi ya mienendo ambayo dini inakataza.

Sheikh Jalala alisisitiza kuwa: Jamii inapaswa kuwa macho na kuchukua hatua za malezi, elimu na uelekezaji wa vijana, huku akionya kuwa endapo juhudi za pamoja hazitafanyika, huenda siku zijazo jamii ikakabiliwa na mabadiliko makubwa katika mitazamo na mifumo ya kijamii kuhusu masuala hayo.

Alieleza hofu yake kwamba hali hiyo inaweza kufikia hatua ya makundi yanayotetea ushoga na usagaji kutambuliwa rasmi nchini, huku watu wakihofia au kukosa nafasi ya kutoa maoni na kukemea mambo yanayopingana na misingi ya imani zao.

Awaomba wazazi na jamii kushirikiana katika kuwalinda vijana

Akihitimisha khutuba yake, Sheikh Jalala alisisitiza umuhimu wa jamii kushirikiana katika kuimarisha malezi ya watoto na vijana, huku akieleza kuwa jukumu hilo haliwezi kuachwa kwa wazazi au walimu pekee, bali linahitaji ushirikiano wa familia, viongozi wa dini, walimu na jamii nzima.

Mwisho wa khutuba yake alimuomba Mwenyezi Mungu awalinde vijana na mabinti, awaepushe na mabalaa, mitihani na mienendo mibaya, na awajaalie wakue katika imani, uchamungu na maadili mema.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha